Pages

Wednesday, July 17, 2013

SHABIKI ALIKIMBIZA BASI LA ARSENAL




Shabiki mmoja raia wa Vetnam jana alifanya kitendo cha ajabu baada ya kukimbia sambamba na basi lilowabeba wachezaji wa Arsenal kwa takribani maili 3.


Katika kulikimbilia basi hilo alikutana na vigingi tofauti lakini kijana yule wa kivetnam hakukata tamaa ya kulifikia basi la Arsenal na kuwaona wachezaji wa timu aipendayo.

Baada ya kulikimbiza basi hilo kwa muda mrefu hatimaye kijana huyo alipata msaada kutoka kwa mwenye pikipiki na kuufikia mlango wa basi hilo na wachezaji wa Arsenal wakamfungulia mlango kisha kumpokea kwa furaha.

Kijana huyo alitimiza ndoto yake baada ya kupiga picha na wachezaji wote pamoja na kocha  Arsene Wenger.

ALCANTARA RASMI BAYERN MUNCHEN APEWA NAMBA 6



CAVANI RASMI MALI YA PSG




NAENDELEA KUBAKI NOU CAMP


Siku chache baada ya kumkosa Thiago Alcantara inaonekana sasa Manchester United ipo njiani kumkosa mchezaji mwingine kutoka FC Barcelona, Cesc Fabregas. Hii inakuja baada ya kocha wa klabu hiyo  Tito Vilanova kusema kwamba ameongea na kiungo huyo wa Spain na ameambia na mchezaji huyo kwamba anahitaji kuendelea kubaki Camp Nou.

Jana jumatatu iliripotiwa kwamba United walituma ofa ya kwanza ya kiasi cha £25.9 million  kwa ajili ya kumsajili Fabregas, ambaye amefeli kupata nafasi katika kikosi cha kwanza tangu aliporudi akitokea Arsenal.

Lakini akiongea na waandishi wa habari leo mchana, Vilanova amesema wazi kwamba Fabregas bado anataka kubaki kwenye klabu yake hiyo ya utotoni, na hana mawazo ya kuondoka kwa sasa.
 "Ninafahamu kwamba tumepokea ofa kadhaa kutoka kwa vilabu tofauti. Niliongea na Cesc na ameniambia kwamba anataka kubaki.

"Cesc hana mawazo ya kuondoka kwenda klabu nyingine. Anajua ushindani ni mkubwa hapa na ana ndoto za kuendelea kuwa hapa na kufanikiwa.

Tuesday, July 16, 2013

OKWI ATOROKA TUNISIA



ETOILE du Sahel ya Tunisia inakusuduia kumshitaki mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa kuingia mitini katika klabu hiyo.
Okwi hajaonekana katika klabu hiyo kwa zaidi ya siku 30, na amekuwa akionekana akirandaranda katika mitaa ya jiji la Kampala, Uganda bila wasiwasi wowote.
Klabu hiyo ilimruhusu Okwi kujiunga na timu yake ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia, lakini tangu wacheze mechi dhidi ya Angola mjini Kampala Juni 15, mwaka huu, mshambuliaji huyo ameshindwa kurejea Tunisia na hajatoa taarifa yoyote.
Etoile du Sahel katika barua waliyomuandikia Okwi Julai 12 mwaka huu (Ijumaa iliyopita) na kusainiwa na Katibu Mkuu, Adel Ghith inasema kuwa iwapo straika huyo angekuwa hajarejea mpaka jana Jumatatu ingempeleka katika  vyombo husika vya sheria kwa hatua zaidi.
Katika barua hiyo, ambayo Mwanaspoti inayo, Katibu Mkuu wa Etoile du Sahel amemwambia Okwi kuwa licha ya kupigiwa simu mara kwa mara na makocha wa klabu hiyo tangu Juni 23, mchezaji huyo ameshindwa kuonyesha ushirikiano wowote.
“Ukiwa kama mchezaji profesheno, matendo yako yanachukuliwa kama kushindwa kuheshimu majukumu yako na ni kwenda kinyume na mkataba wako na klabu,” inasema sehemu ya barua hiyo.
Klabu hiyo imemkumbusha Okwi kuwa mkataba wake wa miaka mitatu utakwisha Julai 15, 2016 na kwamba kwa kutoripoti klabuni hapo ni kwenda kinyume na kifungu cha 2, 8 na 16 cha mkataba wake.
Katibu huyo katika barua hiyo amesema Okwi alikuwa amepewa mpaka jana Jumatatu awe ameripoti katika klabu hiyo vinginevyo atachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufikishiwa katika vyombo husika vya kisheria.
Katibu huyo ameandika barua pepe nyingine mwishoni mwa wiki na kumkumbusha Okwi kuwa suala lake litafikishwa katika Shirikisho la Soka Tunisia (FTF) na Fifa.
Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa) nalo limemuandika barua Okwi kumuonya kuhusu kitendo hicho.
“Jambo hili lipo ndani ya mamlaka yako na klabu. Fufa tulikuruhusu kuondoka ili urejee katika klabu yako, tunakusihi uheshimu kanuni za Fifa katika suala hili,” inasema barua iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa Fufa, Edgar Waston Suubi.
Hata hivyo, habari ambazo Mwanaspoti inazo zinadai kuwa Okwi amegoma kujiunga na klabu yake kwa sababu haijamlipa baadhi ya fedha zake za kusaini pamoja na mshahara wa miezi mitatu.
Okwi aliuzwa na Simba kwa dola 300,000 (Sh 480 milioni), lakini klabu hiyo ya Msimbazi haijapata hata senti moja kwa madai kuwa Etoile du Sahel inapita katika kipindi kigumu na kwamba wanaweza kuwalipa Septemba.
Simu ya Okwi ilikuwa imezimwa jana Jumatatu, lakini watu wake wa karibu walisema alikuwa bado mjini Kampala.

YANGA YAMALIZA USAJILI NA OLOYA

 KOCHA wa Yanga, Ernie Brandts ametoa kauli ya mwisho kuwa anataka nafasi moja ya mwisho ya usajili wa wachezaji wa kigeni asajiliwe, Moses Oloya wa Uganda.
Ingawa amekiri kuwa amesikia mchezaji huyo anahitaji pesa nyingi lakini mambo yote amemwachia mkuu wake ambaye ni Mwenyekiti Kamati ya Usajili wa Yanga, Abdallah Bin Kleb.
Oloya ambaye anakipiga klabu ya Saigon Xuan Thanh, anatakiwa kwa udi na uvumba na Simba.
Na Oloya alipofanya mazungumzo na Mwanaspoti kutoka Vietnam alisema anamalizana na bosi wake wa Saigoni amkubalie aje Simba kabla ya mkataba wake kumalizika Oktoba wakati klabu hiyo ikiwa imebakiza mechi tano, lakini sasa Brandts kaagiza Yanga wafanye vurugu na kumleta kiungo huyo mshambuliaji Jangwani.
Akizungumza na Mwanaspoti jana Jumatatu, Brandts alisema: “Oloya ndiye mchezaji ninayemuhitaji kwa sasa, kawaida napenda mchezaji mzuri kama yeye ingawa nimesikia anahitaji pesa nyingi sana.
“Yanga hatuna tatizo sana kwa sababu kwa sasa, Kiiza (Hamis) amekuja na hawa wengine tulionao mambo yataenda vizuri,”
“Kama tutampata, Oloya tutamaliza kila kitu ingawa mambo hayo yote mkuu wangu, Bin Kleb ndiye anayeyafanyia kazi na anajua tutafanya nini,”alisisiza Brandts ambaye kwa sasa anao wachezaji Mrundi Didier Kavumbagu, Wanyarwanda Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite na Hamis Kiiza wa Uganda, ambaye alikuwa dakika za mwisho kumalizana na Yanga, hivyo kubakiwa na nafasi moja ya mchezaji wa kigeni.
Alipoulizwa kama atamkosa Oloya ni mchezaji wa aina gani anayemuhitaji, Brandts alisema kwa sababu hajajiunga na timu yoyote bado, hawezi kuzungumzia zaidi.
Kwa upande wa kambi ya Simba awali, Mwenyekiti Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe alisema wameshamalizana na Oloya na wamemwacha uhuru yeye mwenyewe amalizane na Saigoni ili atue Simba kabla ya msimu wa Ligi Kuu Bara kuanza.
Oloya mwenyewe alipozungumza na Mwanaspoti hivi karibuni alisema kuwa mipango yake ilikuwa ni kwenda Simba na akakiri kuwa amewahi kufanya mazungumzo na Yanga, lakini alikuwa amefika mbali zaidi na klabu ya Msimbazi kimazungumzo.
Hata hivyo, wachezaji hubadilika kama kinyonga, na ndio maana Mbuyu Twite alisaini mkataba wa Simba kabla ya kuruka kimanga na kutua Jangwani, hivyo suala la Oloya ni jambo la kusubiri mpaka dakika ya mwisho kujua atacheza Jangwani au Msimbazi.
Kocha wa Yanga ana historia katika ulimwengu wa soka akiwa anacheza beki ya kati ya taifa lake la Uholanzi alifunga mabao mawili kwenye mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 1978 dhidi ya Italia, alifunga na kujifunga katika mechi hiyo hivyo matokeo kuwa 1-1.
Katika hatua nyingine, Brandts amezungumzia kambi ya kikosi chake na kusema anahitaji kambi nyingine ambayo atapata uwanja wenye sehemu nzuri ya kuchezea iwe ndani au nje ya nchi.
Alisema pia katika ziara ya Kanda ya Ziwa amepata mazoezi ya kutosha baada ya kucheza na Express wakatoa sare ya 1-1 kabla ya kufungwa 2-1 na baadaye wakatoka suluhu na Rhino ya Tabora.
“Hakuna tatizo kwenye kikosi changu ingawa kwa Tabora mazingira ya uwanja ndiyo hayakuwa mazuri,” alisema Brandts na kusisitiza washambuliaji wake ni wazuri ingawa wanakosa umakini kwenye kufunga.
Yanga haina mpango wa kuwachukua Kabange Twite na Yaw Berko katika usajili wa msimu huu, badala yake inataka straika

WAPINZANI WA USAIN BOLT WAKUTWA NA HATIA YA KUTUMIA MADAWA YA KUONGEZA NGUVU



Wanariadha wawili kati ya wanariadha wenye kasi kubwa duniani Tyson Gay, kutoka Marekani na Asafa Powell wa Jamaica -- wamepatikana na kosa kutumia madawa ya kusisimua misuli.

Gay, ambaye ni mwanariadha wa pili kwa kuwa na kasi kubwa ya kukimbia katika mbio za mita mia moja, amesema anajiondoa kwenye mashindano ya dunia ya riadha yanayotarajiwa kufanyika mjini Moscow mwezi ujao.

Asafa Powell, ambaye alishikilia rekodi ya mbio za mita 100 hadi ilipovunjwa na Usain Bolt mwaka 2008, amekanusha kuwa alitumia dawa hizo makusudi.

Mwanariadha mwenzake wa Jamaica Sherone Simpson pia amepatikana na hatia ya kuzitumia dawa hizo za kusisimua misuli

EDINSON CAVANI ATUA PARIS KUFANYA VIPIMO VYA KUJIUNGA NA PSG


Cavani ametua rasmi jijini Paris Ufaransa tayari kufanyiwa vipimo vya afya baada ya Napoli kukubali ofa £55million kutoka kwa PSG. Endapo mchezaji huyo atafaulu vipimo basi atajiunga na PSG rasmi mapem kesho.

Sunday, July 14, 2013

THIAGO ALCANTARA AJIUNGA NA BAYERN MUNICH



Hatimaye kiungo wa kimataifa wa Spain na FC Barcelona Thiago Alcantara ameuzwa rasmi kwenda kujiunga na mabingwa wa ulaya na Ujerumani Bayern Munich.

Thiago ambaye alikuwa akihusishwa mno na kujiunga na Manchester United ingawa juzi kocha David Moyes alisema hawakuwahi kusema wanamhitaji mchezaji, amejiunga rasmi ya Bayern Munich kwa ada ya uhamisho wa 25 million euros.

Mapema wiki iliyopita kocha wa Bayern Munich Pep Guardiola alikaririwa akisema kwamba anamhitaji Thiago kwenye timu yake na amewaomba viongozi wake kumsajili mchezaji huyo tu msimu huu.

Thiago amesaini mkataba wa miaka minne kuichezea Bayern Munich

STARS HAKIJAELEWEKA BADO CHANI

Wachezaji wa Taifa Stars wakiondoka katika uwanja wa Taifa , Dar es Salaam jana vichwa chini 

Mfupa wa Waganda bado mgumu kwa Taifa Stars. Ni baada ya jana timu hiyo ya Tanzania kushindwa kufurukuta mbele ya wageni wao kwenye mchezo wa kwanza wa kufuzu kushiriki fainali za Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) kufuatia kipigo cha bao 1-0.
Kwa matokeo hayo, Stars inahitaji miujiza kushinda mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo kwenye uwanja ambao utaamuliwa baadaye na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kati ya Namboole au Nakivubo.
Katika mchezo huo kwenye Uwanja wa Taifa, Taifa Stars ilitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza na kuwapa wakati mgumu Uganda, lakini cha kusikitisha ni washambuliaji wake kukosa magoli yasiyo na idadi.
Bao pekee la Uganda lilifungwa dakika ya 46 kupitia kwa Iguma Dennis aliyemfunga kipa Juma Kaseja kwa shuti la pembeni ya lango akimaliza pasi ya shambulizi la kushtukiza kutoka kwa Mpande Joseph.
Kwa matokeo hayo, Stars inaendelea kuwa mteja wa The Cranes, na sasa ili isonge mbele itahitaji ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya marudiano.
Washambuliaji, John Bocco, Amri Kiemba, Mrisho Ngassa waliinyima Stars mabao mengi ya hasa kipindi cha kwanza walichotawala sehemu kubwa ya mchezo.
Uganda waliokuwa wakitumia nguvu nyingi kufika lango la Stars, hawakupata nafasi nyingi za kufunga, lakini nafasi moja waliyoipata ambayo haikuonekana kuwa ya hatari, ndiyo iliyowapa bao pekee.
Stars walikuwa wa kwanza kupiga hodi lango la Uganda dakika ya kwanza, baada ya krosi ya John Bocco kushindwa kuunganishwa wavuni na Amri Kiemba aliyekuwa kiasi cha mita tano kutoka langoni.Mrisho Ngassa aliyekuwa akiwakimbiza vizuri Waganda, alifanya makosa kama ya Kiemba baada ya kushindwa kutikisa nyavu dakika ya 20 kufuatia pasi ya Bocco, ambaye naye dakika moja kabla alikosa bao la wazi.
Taifa Stars waliendelea kuwanyong’onyesha mashabiki wake baada ya kushindwa kufunga kupitia kwa Bocco katika dakika 21 na 23, na baadaye dakika tatu Ngassa naye alikosa bao la wazi.
Shambulizi kubwa la The Cranes lilikuja dakika za 30 na 39, ambapo wangeweza kufunga mabao kama siyo nafasi hizo kupotezwa na Edema Patrick.
Pamoja na Kocha wa Stars, Kim Poulsen kusema bado kuna nafasi ya kushinda mchezo wa marudiano na kufuzu kwa michuano hiyo, matumaini ni kidogo.
Akitetea wachezaji wake kupata nafasi nyingi na kushindwa kufunga, Kim alisema: “Katika soka kukosa mabao ni jambo la kawaida, bado tunaweza kushinda kwenye mchezo wa marudiano.” Kocha wa Uganda, Sredojevic “Micho” Milutin alisema wachezaji wake walicheza kwa kujituma na ndiyo maana wakapata ushindi ugenini.

SHIBOLI MOTO WA KUOTEA MBALI HUKO ZANZIBAR:

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba ya Dar es Salaam, Ali Shiboli ameisaidia timu yake ya Jamhuri ya Pemba kupata pointi moja dhidi ya Bandari ya Unguja. Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Zanzibar uliochezwa juzi Alhamisi kwenye Uwanja wa Gombani, Chakechake timu hizo zilifungana bao 1-1. Shiboli hilo ni bao lake la tatu katika mechi tatu mfululizo ambazo Jamhuri zimecheza katika ligi hiyo inayoelekea ukingoni. Mshambualiji huyo alifunga mabao yake wakati Jamhuri ilipoichapa Malindi mabao 3-1, ilipofungwa na KMKM mabao 3-2 na ilipotoka sare ya 1-1 na Bandari. Shiboli aliyeichezea Simba na baadaye kuuzwa kwa mkopo anaonyesha kuwa amerejea katika kiwango chake kizuri cha kupachika mabao wavuni kilichomfanya wakati fulani azigonganishe Simba na wapinzani wake wa jadi, Yanga. Timu zote hizo mbili zilipigania kumsajili mchezaji huyo baada ya kuonyesha makali akiwa timu ya soka ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) na Simba ndiyo waliofanikiwa kunasa saini yake

MAN UNITED NJIANI KUMPOTEZA THIAGO ALCANTARA


MANCHESTER UNITED wapo njiani kupoteza nafasi ya kumsaini mchezaji wa Barcelona Thiago Alcantara baada ya kocha wa Bayern Munich Pep Guardiola kusema kwamba: “Namtaka Thiago hapa Bayern Munich.” Kiungo huyo mwenye miaka 22 amekuwa kwenye tetesi za kuhusishwa kujiunga na United kwa muda mrefu sasa.
Lakini sasa anaweza akabadili mawazo na kwenda kujiunga na kocha ambaye alimtambulisha kwenye soka la kimataifa wakati akiwa na Barca.
Guardiola alisema: “Namataka Thiago Alcantara. Nimewaambia Bayern wafanye kila kitu kumsajili lakini sijui nini kitatokea.
“Thiago ni mchezaji pekee ninayemhitaji, hilo ndilo nililowaambia.
“Nimsajili yeye au nisisajili kabisa. Tuna wachezaji wengi lakini tunahitaji ubora wa ziada ambao Thiago Alcantara atauleta.
“Namfahamu Thiago vizuri sana. Nimeongea na mwenyekiti Rummenigge na mkurugenzi wa ufundi Sammer kuhusu kumsajili, sasa tusubiri tuone nini kitatokea.
“Sidhani kuongeza kiungo mwingine kutaleta tatizo kwetu. Nimeongea na klabu kuhusu mpango/wazo wangu na sababu za kumhitaji Thiago.
“Nimewapa mawazo yangu, ;alini naisikiliza bodi itasemaje. Wakikataa pia ni sawa.”

MKUTANO TFF WAPITISHA MAREKEBISHO YA KATIBA



Mkutano Mkuu Maalumu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) uliofanyika leo (Julai 13 mwaka huu) umepitisha marekebisho ya Katiba yake, hivyo mchakato wa uchaguzi unatarajia kuanza wakati wowote.
Wajumbe zaidi ya 100 walihudhuria Mkutano huo uliofanyika ukumbi wa NSSF Waterfron, Dar es Salaam na kufunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera aliyewataka wajumbe kuhakikisha kiwango cha mpira wa miguu nchini kinakuwa.
Mkutano huo uliokuwa chini ya uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga umefanya marekebisho ya Katiba kutokana na maelekezo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). James Johnson kutoka Idara ya Wanachama ndiye aliyeiwakilisha FIFA katika mkutano huo.
Aprili mwaka huu FIFA ilisimamisha mchakato wa uchaguzi wa TFF, na kuagiza kwanza yafanyike marekebisho ya Katiba ili kuingiza Kamati ya Maadili, na Kamati ya Rufani ya Maadili ambavyo ndivyo watashughulikia matatizo ya kimaadili kwa familia ya mpira wa miguu nchini.
Mbali ya kamati hizo, mabadiliko hayo pia yametengeneza ngazi mbili za kushughulikia masuala ya kinidhamu ambazo ni; Kamati ya Nidhamu na Kamati ya Rufani ya Nidhamu.
Kamati ya Utendaji ya TFF chini ya Rais Tenga itakutana kesho (Julai 14 mwaka huu) kwa ajili ya kuteua wajumbe watakaounda Kamati hizo ili kuruhusu kuanza mchakato wa uchaguzi ambao FIFA iliusimamisha hadi vitakapoundwa vyombo hivyo.

KOCHA ANENA STRAIKA SIMBA NA BEKI YANGA


KOCHA Mkuu wa Rhino ya Tabora, Renatus Shija amezichambua Simba na Yanga, baada ya timu hizo za Dar es Salaam kucheza na timu hiyo katika mechi za kirafiki wiki iliyopita.
Simba iliifunga Rhino mabao 3-1 kabla ya timu hiyo ya Tabora kutoka suluhu na Yanga katika mchezo uliofuata.
Akizungumza na Mwanaspoti, Shija alisema: “Washambuliaji wa Simba, ni wazuri mmoja mmoja, lakini wana uwezo binafsi na wazuri kwenye umaliziaji kwani anapotafuta bao anapambana mpaka mwisho kuhakikisha anafanikiwa.”
“Yanga wanao washambuliaji wengi wanaofahamika kwa majina, wanacheza vizuri lakini hawana uwezo binafsi, mbinu za mmoja mmoja katika umaliziaji hawana na wanapoteza nafasi nyingi za mabao,”alisema Shija.
Simba walishinda mabao 3-1, mawili yakifungwa na Edward Christopher na Said Nassor ‘Cholo’.
Safu ya ushambuliaji ya Simba iliundwa na Msudani Kun James, Betrem Momboki, Zahoro Pazi na Ramadhani Singano ‘Messi’ wakatoka na kuingia Ismail Rashid, Edward Christopher, Sino Agustino na Marcel Kaheza.
Wakati Yanga ilikuwa na Mrundi Didier Kavumbagu, Said Bahanuzi, Jerry Tegete akatoka akaingia Shaaban Kondo na Hamis Thabit akatoka akaingia Abdallah Mguli.
“Kwa upande wa mabeki, Yanga ni wazuri sana,” alisema Shija ambapo katika mchezo huo Yanga ilikuwa na Mnyarwanda Mbuyu Twite, Rajab Zahir akatoka na kuingia Ibrahim Job pembeni kulikuwa na Oscar Joshua na Juma Abdul licha ya kuwa mabeki wake mahiri wa kikosi cha kwanza, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Devid Luhende wapo na Taifa Stars.
Na Simba ilikuwa na Cholo, Samwel Ssenkoomi na Asuman Buyinza akatoka akaingia Mussa Mudde wote raia wa Uganda, Omary Salum akatoka akaingia, Haruna Shamte.
Shija alichambua pia kwenye kiungo na kukimwagia sifa kikosi cha Msimbazi: “Simba ilikuwa nzuri kwenye kiungo zaidi ya Yanga, wanacheza kwa ushirikiano katika kuzuia na kushambulia pia.”
Kiungo ya Simba ilichezwa na Jonas Mkude na Mcongomani Kuipou Felix wakati Yanga ni Salum Telela na Nizar Khalfan.
Hata hivyo huenda kiungo ya Yanga ilishindwa kutamba kutokana na sehemu kubwa ya wachezaji  wanaocheza nafasi hiyo kama, Mnyarwanda Haruna Niyonzima kutokuwa na timu, Athuman Idd ‘Chuji’, Frank Domayo na Simon Msuva wako na Taifa Stars.

MANCHESTER CITY YAPANDA DAU KWA RONALDO


MANCHESTER City imeanzisha vita mpya na majirani zao Manchester United baada ya kutangaza wameingia kwenye mbio za kumnasa mpachika mabao wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo.
Manchester City ipo tayari kutumia kiasi kikubwa cha fedha kumsajili staa huyo wa zamani wa Manchester United.
Mmiliki wa klabu sasa hataki mchezo na yupo tayari kutoa dau kubwa iwezekanavyo na ameahidi kutoa mshahara wa pauni 300,000 kwa nyota huyo iwapo atakubali kutua Etihad.
Kwa miezi mitano, Manchester United imekuwa ikijaribu kumshawishi mchezaji huyo mwenye miaka 28 bila ya mafanikio na hawajakata tamaa, wanaendelea kumshawishi.
Man City wanafahamu kuwa vita hiyo ni kali lakini wanaamini fedha ndiyo fimbo muhimu. Viongozi wa Manchester City wanaishawishi Real Madrid imweke sokoni mchezaji huyo na kama wakikubali jambo hilo, watatoa kiasi kikubwa cha fedha.
Mmiliki wa Man City, Sheikh Mansour amewaambia viongozi wa juu wa klabu kuwa wanatakiwa kufanya kila liwezekanalo kumnasa nyota huyo ili kushtua dunia.
Ronaldo amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake na bado hajasaini mkataba mpya. Tayari viongozi wa Manchester City wamewasiliana na wakala wa Ronaldo, Jorge Mendes kwa ajili ya dili hilo.

ROONEY AUMIA MAZOEZINI AHOFIA KUBAKI OT


HUENDA maisha ya Wayne Rooney yakazidi kuwa kwenye utata katika kikosi cha Manchester United. Skendo inayoendelea juu ya mchezaji huyo ni suala la kutaka kuondoka kwenye klabu yake huku kocha David Moyes akijitahidi kumtuliza, lakini huenda nyota huyo akapata nafasi ya kutuliza kichwa na kujipanga upya kufuatia kuumia misuli na kuenguliwa kwenye ziara ya mechi za kirafiki huko Bangkok, Thailand.
Mchezaji huyo alikuwa kwenye kundi la wachezaji na viongozi wa Man United wapatao 200 waliosafiri umbali wa maili 5,961 kwa saa 11 kutoka jiji la Manchester kwenda Bangkok, Thailand lakini baada ya kufanya mazoezi kwa kwa nukta chache tu, nyota huyo aliumia na hivyo kurudishwa jijini Manchester.
Kwa maana hiyo Rooney alisafiri umbali wa maili 11,922 kwa saa 22. Rooney alitulia kwa saa 16 pekee akiwa Bangkok na kuanza safari mpya.
Rooney aliwaambia mashabiki kwenye Facebook: “Nimesikitika kwa kuumia, nilikuwa mwenye afya njema na mazoezi yalikuwa yakienda vizuri.”
Baada ya kupata maumivu hayo, Rooney alirudi jijini Manchester kukutana na madaktari kwa uchunguzi wa kina.
Taarifa ya awali juu ya tatizo la Rooney ilisema: “ Uchunguzi wa awali unaonyesha mchezaji huyo ameumia. Viongozi wameamua mchezaji huyo arudi nyumbani kwa ajili ya uchunguzi zaidi. 
“Kuna uwezekano mkubwa mchezaji huyo asiingie uwanjani kwa mwezi mmoja. 
Kwa maana hiyo, Rooney atakuwa akitazamwa kwa karibu na madaktari wa klabu kwa muda wa wiki mbili na baada ya hapo ataanza mazoezi mepesi. Huenda mchezaji huyo akacheza mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya Wigan Agosti 11. 
Hata hivyo mchezaji huyo bado hajaamua iwapo atabaki kwenye klabu hiyo au la na imefahamika kuwa anaweza kutumia muda huo kutafakari kwa kina juu ya maisha yake ya baadaye.
Kocha wa Manchester United, David Moyes amesema Rooney hauzwi kwa njia yoyote. 
“Nimekutana na Wayne Rooney mara nne, naamini atabaki kwenye klabu hii. 
 “Kuna mambo mengi yamesemwa juu yangu na Wayne, lakini mimi na Rooney tuna uhusiano mzuri, huwa tunatembeleana. Huwa anafika nyumbani kwangu na mimi nakwenda kwake. Sina uhasama na mchezaji huyo.”

YAYA TOURE TAJIRI MWENYE HOFU YA MUNGU


BINADAMU wengi wana tabia ya kulewa sifa na hupenda maisha ya kifahari hasa wanapopata fedha nyingi.
Lakini hali ni tofauti kwa mwanasoka nyota wa Ivory Coast, Yaya Toure, ambaye licha ya kuingiza Pauni 18 milioni kwa mwaka, hajabadilisha staili ya maisha yake.
Mchezaji huyo ambaye amelelewa kwenye maadili ya dini ya Kiislamu, amewahi kusema imani yake ndio inamfanya asijione tofauti na watu wengine licha ya kuwa na fedha nyingi.
Toure ambaye ndugu zake wawili; Kolo na Ibrahim, nao pia ni wanasoka, amewahi kuanika kuwa hawezi kusahau asili yake. Jambo hilo ndilo linafanya awe na kawaida ya kutoa vifaa vya michezo kwa vijana wadogo katika nchi yake na pia kuisaidia familia yake kwa hali na mali.
“Ninapokuwa mbali na nyumbani, jambo ambaloo huwa nalikumbuka mara zote ni watu wa mji wangu,” alisema.
Maneno yake yanaonyesha jinsi ambavyo mchezaji huyo hajali maisha ya fedha, anaangalia utu kwanza. Gazeti la Time lilimtaja mchezaji huyo kushika namba 15 kwa utajiri miongoni mwa wachezaji wa England.
Mchezaji huyo anashika namba moja kwa kipato kikubwa miongoni mwa wanasoka wa Afrika kwa sasa.
Aliposaini mkataba wa miaka minne wenye thamani ya Pauni 24 milioni katika klabu yake Aprili mwaka huu, mshahara wake umemfanya awe kwenye ramani ya wachezaji matajiri.  Awali mchezaji huyo alikuwa akilipwa Pauni 200,000 kwa wiki, lakini baada ya kusaini mkataba mpya, mshahara wake umekuwa Pauni 240,000 kwa wiki.
Mkataba huo utamfanya aishi Manchester City mpaka mwaka 2017 ambapo wakati huo atakuwa na umri wa miaka 34.
Gazeti la Forbes limemtaja mchezaji huyo kuwa ameshika nafasi ya 67 kwa utajiri miongoni mwa wanamichezo wote duniani.
Ukiachilia mbali matangazo mbalimbali, nyota huyo huweka kibindoni Pauni 5 milioni kila mwaka kwa kipato cha klabuni pekee
Mchezaji huyo ameingia mikataba na makampuni mbalimbali ya matangazo ya jezi, viatu na haki ya picha ambapo kwa pamoja inamfanya apate Pauni 11 milioni kwa mwaka.
Vile vile anapata Pauni 823,000 kila wakati Manchester City inapotua kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ingawa mchezaji huyo hapendi makuu, hivi karibuni alinunua gari aina ya Porsche ya rangi nyeupe ambalo hulitumia kuzungukia kwenye shughuli zake. Gari hilo lina thamani ya dola 82,050. 
Licha ya kuwa na magari yenye thamani kubwa, anaishi kwenye jumba la kifahari pia huko Cheshire, nyumba hiyo ina thamani ya Pauni 1 milioni.
Mwanzoni mwa mwaka huu ilidaiwa kuwa nyumba ya mchezaji huo ilishika moto, hata hivyo kitengo cha zimamoto kiliwahi kufika eneo la tukio na hakukuwa na madhara makubwa yaliyotokea.
Baba yake alonga
Baba yake (Mory Toure) aliwahi kusema kuwa anamshukuru Mungu kwa kipato cha mtoto wake ambacho kimewaondoa kwenye lindi la umasikini.
Mory mwenye umri wa mika 66, ambaye alikuwa mwanajeshi kabla ya kustaafu, aliwahi kusema: “Kabla watoto wangu (Yaya, Ibrahim na Kolo) hawajawa nyota katika soka, tulikuwa masikini mno.
“Hatukuwa na uhakika hata wa chakula. Watoto hawakuwa na mipira ya kuchezea na mavazi yalikuwa ya taabu. Lakini Kolo na Yaya wameleta mapinduzi makubwa.”
Asilimia 42 ya wananchi wa Ivory Coast wanaishi kwenye umasikini wa kutupwa. “Nafahamu fedha haziwezi kumfanya mtoto wangu abadili staili ya maisha. Nadhani fedha hizo zitatumika kumfuta machozi baada ya kufiwa na mama yake (Tocontoio) wakati alipokuwa na umri wa miaka 19,” aliongeza baba huyo.
“Ninafahamu hata mke wake (Gineba) anajua nini cha kufanya, hata yeye anaongozwa na sheria za Kiislamu.”
Licha ya kusaidia familia yake, mchezaji huyo anasaidia pia  kukuza soka la Ivory Coast na sehemu kadhaa za Afrika Magharibi
Mwaka 2011 aliingia mkataba na kampuni ya vifaa vya michezo ya Puma kwa ajili ya kusaidia chipukizi wa Ivory Coast.
Klabu alizochezea
Yaya Toure aliondoka Ivory Coast akiwa na umri wa miaka 18 na kuanza soka la kulipwa katika kikosi cha Waasland-Beveren ya Ubelgiji baadaye akatua FC Metalurh Donetsk ya Ukraine kisha akaenda Olympiacos F.C. ya Ugiriki.
Baada ya hapo akachezea AS Monaco ya Ufaransa, hata hivyo mchezaji huyo hakuwa akilipwa vizuri mpaka alipotua Barcelona mwaka 2007. Mwaka 2010 akatua Manchester City ambapo mshahara wake ulipanda maradufu.

NAKWENDA NJE SHOMARI KAPOMBE

Shomari Kapombekushoto  na Gevinho 

HABARI zilizopo Dar es Salaam ni kwamba kiraka wa Simba na Taifa Stars, Shomari Kapombe ameingizwa mkenge kwenye safari yake ya kufanya majaribio barani Ulaya.
Baadhi ya wadau wamedai wakala anayetaka kumpeleka mchezaji huyo ni magumashi na kwamba klabu zinazodai kumtaka hazina mpango naye.
Baadhi ya watu wamenukuliwa wakidai kuwa wakala huyo ni Mtanzania ambaye ametumia ujanja wa kidigitali kumhadaa Kapombe.
Lakini, Kapombe mwenyewe ameitamkia Mwanaspoti kwa kujiamini kuwa yanayozungumzwa mtaani dhidi yake na wakala huyo ni uzushi na kwamba ukweli anao yeye na ndio huu anaoueleza hapa.
Kapombe anasisitiza kuwa hakuwahi kuzungumza na chombo chochote cha habari kuhusiana na safari hiyo na kudai kuwa baadhi wamekuwa wakimlisha maneno. 
Mchezaji huyo ameionyesha Mwanaspoti tiketi yake ya safari na nyaraka zote za safari hiyo ya Uholanzi Ijumaa ijayo na tayari ameshalipiwa gharama mbalimbali na wakala huyo aliyemtambulisha kwa jina la Dionis Kadito ‘Denison’.
“Tayari amelipia gharama za safari ikiwamo tiketi ya kusafiria, visa na mambo mengine na pia ameahidi kugharamia kila kitu nitakapokuwa Uholanzi.”
WALIVYOJUANA
Kapombe amelieleza Mwanaspoti kuwa aliwahi kumsikia wakala huyo kabla ya mwaka jana kukutana naye katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwenye moja ya mechi za Simba katikaLigi Kuu Bara.
 “Nilikutana kwa mara ya kwanza mwaka jana na wakala huyu hapa Dar es Salaam na aliniomba tuzungumze kuhusu kufanya majaribio nje ya nchi,” anasema.
“Licha ya kuwa na ndoto siku moja kucheza soka la kulipwa, nilitilia maanani walichoniambia kaka zangu kina Boban (Haruna Moshi) kuwa niwe makini na mawakala wanapokuja, hivyo nikaona nimfuate mzee wangu wa karibu ambaye ndiye aliyenisaidia Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua) kilichopo Morogoro,  Profesa Madundo Mtambo ambaye nilimueleza na nikamwomba anisaidie kujua kamaDenison alikuwa ni wakala mwenye malengo chanya ya kunisaidia au la.
“Nakumbuka Profesa Mtambo alifanya naye mawasiliano huku mimi nikiwa kimya na sifanyi naye mawasiliano ndipo Profesa huyo ambaye ni kama baba kwangu aliponiambia kuwa wakala huyo ni wa kweli, nimezungumza naye sana na nimefuatilia nyendo zake na kujua kazi yake kwa ukaribu na ni mtu aliyewasaidia vijana wengine kupata timu nchi za Ulaya hususani Uholanzi na Ufaransa,” alisema Kapombe akimnukuu Profesa huyo
Kapombe anasema kuwa aliamua kumtumia Profesa huyo kwa kuwa amekuwa mshauri wake kwa muda mrefu na amekuwa mpenzi mkubwa wa soka lake.
Profesa Madundo Mtambo ni mwanasoka msomi na pia mshambuliaji  nyota wa zamani wa klabu ya Reli ya Morogoro na ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine.
WAKUTANA TENA MOROCCO
Kapombe anaeleza kuwa baada ya kuambiwa na Profesa Mtambo kuwa anaweza kufanya mazungumzo na wakala huyo, ndipo akaanza kuwasiliana naye kwa ukaribu na akakutana naye tena Morocco akiwa na Taifa Stars.  “Tulipokwenda Marrakech, Morocco tulikutana na tulizungumza na nikamweleza kuwa sitoweza kwenda kwa wakati huo. Akanionyesha makabrasha mbalimbali yakiwemo rekodi zake za fedha, barua kutoka Manispaa ya Jiji ya huko Uholanzi ambayo ni ya kumsaidia kutafuta visa ya kukaa katika nchi hiyo.
“Pia aliambatanisha taarifa za mtaalamu wa ufundi, ambaye huwapima wachezaji na kuwasaidia kuwa fiti kabla hawajapeleka katika timu mbalimbali.”
TIMU ANAZOENDA
Kapombe anasema kuwa amekuwa akisikia watu wakisema anakwenda FC Twente, lakini wakala huyo alimwambia asiwe na papara akifika huko ndipo atajua ni wapi atampeleka kufanya majaribio.
“Mimi kwa kweli sijui timu kwa jina ambayo nitaenda kufanya majaribio zaidi ya wakala huyo ambaye ameniita, ameniambia kuwa kuna timu mbili, zinazoshiriki Ligi Kuu Uholanzi na moja ya Ligi Daraja la Kwanza, mimi nahitajika kuweka juhudi zaidi hivyo timu yoyote itakayovutiwa zaidi kama atakavyosema wakala huyo nitapiga kazi kwani zaidi naangalia maslahi yangu,” anasema  Kapombe.
Dionis Kadito, ambaye ni raia wa Tanzania anayeishi Uholanzi ni wakala wa wachezaji wa soka anayetambuliwa na Chama cha Soka Uholanzi na Shirikisho la Soka la Dunia (Fifa).
Kwa mujibu wa Kapombe na baadhi ya makabrasha yaliyoshuhudiwa na mwandishi wa habari hizi yanaonyesha kuwa Dionis Kadito anamiliki kampuni inayoitwa DFK Voetbal Agent  iliyopo Uholanzi.
SIMBA
Kapombe anasema kuwa mara ya kwanza alipowaeleza klabu ya Simba mchakato huo: “Waliniambia nitulie lakini mwishowe walinipa barua, ambayo ndiyo iliyonisaida kwa ajili ya maandalizi ya safari hiyo kwani bila barua ya Simba ambao ni waajiri wangu nisingeweza kwenda kokote.
“Simba inaonekana walikuwa wanatazama kwa umakini kama dili nililopata litakuwa na manufaa kwangu na kwao kama walezi wangu hivyo nashukuru Mungu walikubali na kunipa baraka zao kufanya majaribio,” anasema Kapombe ambaye amethibitishwa kwamba mkataba wake na Simba unamalizika mwakani Aprili na si Desemba kama ilivyokuwa ikidaiwa awali.
“Nahitaji kucheza nje ya nchi, natamani kucheza ligi nyingine kwani nakusudia kukomaa kiakili na kuwa mchezaji wa kimataifa,”anasema mchezaji huyo ambaye inadaiwa amewaambia Simba kwamba hata kama atabaki atataka kucheza zaidi beki ya kulia au kushoto kwavile ndiko anakomudu zaidi.
Mchezaji huyo wa zamani wa Polisi Morogoro anasema anapenda kucheza na kujaribiwa kwa nafasi za beki wa pembeni (kushoto na kulia) na kiungo mkabaji kwani nafasi za beki wa kati hawezi kuzimudu vizuri kutokana na kimo chake.
“Taifa Stars inanipa faida ya kuonekana, hivyo nafurahi kuwa kocha huwa ananitumia kwenye hizo nafasi ninazozipenda ingawa najua kuwa ninapocheza kati huwa nacheza poa lakini ufupi wangu naona unanipunguzia ubora kwenye nafasi hizo. Pia wakati mwingine mimi kutumika kama kiraka ina faida zake na zaidi inanigharimu kwa sababu nabidi kujibadili binafsi na kuvaa uhusika tofauti tofauti,” anasema
Uongozi wa Simba umesema kuwa mchezaji huyo anakwenda kwenye majaribio kwenye klabu ya FC Twente na hawana habari mpya.

NURDIN BAKARY AFUNGUKA - 'TWITE ALISAJILIWA ILI KUMMALIZA NSAJIGWA, KIIZA ALIPWE ANACHOSTAHILI - KASEJA ANASTAHILI KUENDELEA KUWA NAMBA 1 SIMBA


KIRAKA Nurdin Bakari aliyeachwa na Yanga baada ya mkataba wake kumalizika amefichua siri baada ya kutamka kwamba Mbuyu Twite alisajiliwa na viongozi wa Yanga ili aje kumaliza kipaji cha Shadrack Nsajigwa.
Twite alisajiliwa na Yanga akiwa njiani kutua Simba ambapo mchezaji huyo amekuwa akipendelea sana kucheza beki ya kati lakini imemilikiwa na Kelvin Yondani na Nadir Cannavaro.
Twite alikabidhiwa namba ya Nsajigwa ambaye Yanga imemuonyesha mkono wa kwaheri kwa madai kwamba ameshuka kiwango na tayari Lipuli ya Iringa imemsajili kama kocha.
Nurdin alisema; “Hivi unajua Mbuyu (Twite) ni viongozi waliamua tu kumsajili bila kulishirikisha benchi la ufundi. Ndiyo maana unamwona anachezeshwa beki wa kulia badala ya beki wa kati,”alisema Nurdin aliyewahi kuichezea Simba na AFC ya Arusha.
Lakini viongozi wa Kamati ya Usajili wa Yanga wamesisitiza kwamba mchezaji huyo alikuwa chaguo la kocha Ernest Brandts ambaye amewahi kufanya naye kazi akiwa APR ya Rwanda.
Nurdin alisema baada ya Nsajigwa kutakiwa na Simba msimu wa 2011 na baadaye dili ikashindika alianza kuwekewa mizengwe: “Baada ya Nsajigwa kumalizana na viongozi wa Yanga, tulidhani yameisha. Fitna zilianza na kumletea mabeki wengi kwa lengo la kumshinikiza kocha awe anamweka benchi,” alisema Nurdin na kuongeza kuwa beki wa kwanza aliyesajili kwa nia ya kumpoteza Nsajigwa alikuwa Taita (Godfrey) kutoka Kagera Sugar.
“Lakini alishindwa kumweka benchi, baada ya kuona malengo yao hayajatimia walimletea tena beki mwingine Juma (Abdul) kutoka Mtibwa Sugar na baadaye akaja Mbuyu lengo lao likatimia.”
Nurdin pia amepinga vikali kutemwa kwa straika Hamis Kiiza na kipa Juma Kaseja.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Tabata, Nurdin alisema: “Unajua hawa viongozi wa Simba na Yanga wana chuki zao tu binafsi, mimi bado naamini Kaseja (Juma) ndiye kipa bora kwa Tanzania. Pia, ana nafasi ya kuendelea kuichezea Simba na kwa mafanikio makubwa.”
“Kama unataka kuchukiwa na viongozi wa timu hizi mbili dai chako, kwa jinsi namfahamu Kaseja ni mtu ambaye hataki kuburuzwa. Ni mtu ambaye yupo mstari wa mbele kudai haki yake. Nafikiri ndiyo yaliyomkuta kama ilivyo kwangu.”
“Kaseja bado atabaki kuwa kipa bora na hakuna anaweza kupinga hilo. Sidhani kama atakosa timu ya kuichezea. Ni mtu anayelijenga vizuri jina lake kisoka. Kwa upande wa Kiiza, nafikiri anastahili kudai kuongezwa mshahara na dau la kusaini mkataba mpya anafanya kazi na inayoonekana. Kwanini wanashindwa kuthamini mchango wake na kumpa kile anachostahili,” alihoji.
“Mbona Haruna (Niyonzima) alitaka na kuboreshewa masilahi yake, iweje inashindikana kwa Kiiza mpiganaji, kuna tatizo?  Viongozi wa timu hizi mbili wanachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu maendeleo ya soka katika klabu hizi mbili kubwa. Hawana malengo endelevu,”alisisitiza mchezaji huyo mwenye rasta.

Saturday, July 13, 2013

JUNINHO KUCHEZA BURE VASCO DA GAMA ILI ALIPWE MADENI YAKE YA NYUMA


Mchezaji wa zamani wa Brazil Juninho Pernambucano anatarajia kucheza bure baada ya kurudi kwenye timu ya Vasco de Gama.

Kiungo huyo mwenye miaka 38, ambaye aliwahi kuitumikia klabu hiyo katika vipindi viwili tofauti, anajiandaa kurudi kwa kipindi cha tatu kwenye klabu hiyo yenye maskani yake ya Rio De Jeneiro ambapo hatopata mshahara.

Badala yake, nyota huyo wa zamani wa Lyon ameripotiwa atapokea malipo ya madeni yake yote ya zamani anayoidai klabu hiyo.  

Inaeleweka kwamba Juninho atarudi kujiunga na klabu hiyo ya Brazil kwa miezi sita kabla ya kutundika daluga zake. 

Mapema mwezi huu alimaliza mkataba wake na klabu ya MLS  New York Red Bulls baada ya miezi saba, ambapo alikatisha mkataba wake akitoa sababu binafsi ndio zilizosababisha

DROGBA KUJENGA HOSPTALI TANO NDANI YA IVORY COAST KWA AJILI YA WATOTO NA WANAWAKE


Kupitia taasisi yake ya kutoa misaada, nahodha wa Ivory Coast na gwiji wa Chelsea Didier Drogba atasaidia ujenzi wa kliniki tano za watoto na wanawake katika nchi yake. Tangazo hilo lilitolewa na katibu mkuu wa Didier Drogba Foundation Guy Roland Tanoh, ambaye alisema kwamba ujenzi wa kliniki hizo utafadhiliwa na Taasisi ya London galas pamoja na fedha Drogba mwenyewe.
Kutoka SuperSport:
Tanoh amesema kiasi cha 2.5 billion CFA francs ($5 million) kitatumika kuwekeza katika ujenzi wa kliniki hizo, huku zikijengwa katika miji mitano mikubwa ya nchi hiyo Abidjan, Yamoussoukro, Man, Korhogo na San Pedro.
“Drogba aliendesha mchango huko London na zikapatikana kiasi cha $ 2 billion CFA francs ($4 million),” Tanoh alisema. “Kiasi kilichobakia cha million francs ($1 million) hakitakuwa tatizo kuona ndoto ya mwenyewe Drogba ya kuona afya za wananchi wa Ivory Coast zinapewa kipaumbele.”
Drogba mara ya kwanza alitangaza mpango wake wa kujenga hospitali kubwa katika jiji la Abidjan mwaka 2009 akitumia fedha zote - kiasi cha £3 million ($4.5 million) alicholipwa na Pepsi. Lakini badala ya kujenga hosptali hiyo moja kubwa akaamua ambayo ingekuwa mjini tu, akaamua kujenga vituo vitano vya afya katika mikoa mingine ili kuweza kusambaza vizuri huduma za afya.

MESSI: NINA DENI KWA RONALDINHO



Lionel Messi amefunguka na kusema ana deni kubwa la shukrani kwa Ronaldinho kwa namna alivyoweza kumsaidia wakati anaingia kwenye kikosi cha kwanza cha Barcelona.

Mshindi huyo wa mara wa tuzo ya Ballon d'Or aliingia kwa mara ya kwanza kikosi cha kwanza cha Barca mwaka 2004, mwaka mmoja baada ya Dinho kuwasili Nou Camp akitokea Paris Saint-Germain.

Huu ni wakati Messi anasema hatokuja kuusahau kwenye maisha na anakiri ukarimu wa Ronaldinho pamoja na kuwa staa mkubwa kumliko ulimfanya azoee kwa haraka maisha ya kikosi cha wakubwa cha Barca. 

"Siku zote nimekuwa nikisema, siku tu nilipoingia chumba cha kubadilishia nguo Ronaldinho na wenzie Deco, Sylvinho na [Thiago] Motta walikaniribisha na kunipa baadhi ya vifaa, lakini zaidi ni Ronaldinho ambaye pia alinifundisha vitu vingi uwanjani na nje ya dimba," Messi aliiambia Barca TV"Ulikuwa ni msaada mkubwa. Ni vigumu kuenda kwenye timu ya mastaa kama Ronaldinho na kupata ukarimu kama wake. Alifanya kila kitu kikawa rahisi kwangu. Nilikuwa na bahati kuwa karibu nae na kushea vitu vingi.

"Ninaweza kusema Ron ni mtu mzuri sana na hicho ndio kitu muhimu."
Ronaldinho aliiwezesha Barca kubeba makombe mawili ya Liga na Champions League wakati wa miaka yake mitano aliyoitumikia klabu hiyo ya Camp Nou na Messi anaamini kiungo huyo mwenye miaka 33 ana mchango mkubwa kwa mafanikio aliyonayo sasa.

"Ronaldinho ndio mtu aliyeleta mabadiliko makubwa kwenye klabu hii," anasema. "Klabu ilikuwa inapitia wakati mmoja m'baya sana lakini hali hiyo ilibadilika mara tu alipowasili. Msimu wake wa kwanza hatukushinda chochote lakini watu walimpenda sana. Baadae yakaja mataji na akawapa furaha watu wengi sana

JE TAIFA STARS ITAWEZA KUFUTA UTEJA NA KULIPA KISASI KWA UGANDA KWENYE MICHUANO YA CHAN???



Leo Jumamosi tarehe 13, July: Tanzania itapambana na Uganda kwenye uwanja wa taifa katika mchezo wa kugombea nafasi ya kushiriki kwenye michuano ya mataifa huru ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza kwenye ligi za ndani. 

TAARIFA ZA TIMU YA UGANDA:

Uganda Cranes ilitua Bongo wakitokea kwao siku ya alhamisi. Kikosi cha wachezaji 18 na kufikia kwenye hotel ya Sapphire iliyopo katikati ya jiji la Dar es salaam wakionekana kuwa kwenye hali nzuri kuelekea kwenye mchezo wa leo katika dimba la uwanja wa taifa unaoweza kubeba mashabiki zaidi ya 55,000. 
Uganda wanatarajiwa kuchezesha wachezaji wengi wapya kwenye hatua hii ya kimataifa. Ukimuacha mlinzi Dennis Iguma na kiungo Wasswa Mawanda, ambao walicheza dakika zote 90 kwenye mchezo wa kugombea kwenda Brazil 2014 dhidi ya Liberia na Angola, wachezaji wote waliobakia bado hawajaonja utamu wa soka la kimatiafa. 
Hakuna beki wa kushoto asilia kwenye kikosi hiki cha Micho, ukizingatia mchezaji aliyeitwa kuja kucheza kwenye nafasi hiyo  Habib Kavuma, aliondolewa kikosini baada ya kugundulika kwamba alipewa kadi nyekundu kwenye mchezo wa 2011 CHAN dhidi ya Gabon. Hili linamuacha Micho Akibakiwa na mbadala Yusuf Mukisa, beki wa kulia ambaye hujaribu kucheza nafasi hiyo pia.
Wachezaji wengine ambao wana uzoefu kidogo na michuano ya CHAN ni Ayubu Kisaliita, Patrick Edema, Tonny Odur Hamuza Muwonge, ambao walicheza kwenye michuano ya CHAN iliyofanyika Khartoum, Sudan.
Kutokana kuwa ugenini - Micho anategemewa kuipanga timu yake huku akicheza mchezo wa kuzuia sana na kushambulia kwa kushtukiza. Uganda wanaweza kuanza kwa mfumo wa 4-2-1-3, baadae wakibadilika kuja 4-3-3 na 4-4-2 kadri muda unavyozidi kusogea.


MCHEZAJI WA KUCHUNGWA: Dennis Iguma


Dennis Iguma ameimarika sana kwenye kiwango chake, kujiamini kwake na namna anavyojua kucheza kitimu. Mchezaji huyu ambaye alitumia utoto wake kupata mafundisho ya soka kupita chuo cha soka cha Entebbe, anaweza kucheza popote uwanjani kwa kiwango kile kile anachocheza kwenye nafasi yake ya kawaida. 
Iguma, kwa sasa anaichezea klabu ya Sports Club Victoria University anategemewa kuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa Stars wakiongozwa na Canavaro na Yondani.
TANZANIA:
Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen amemrudisha kikosini beki wa kulia wa Yanga, David Luhende akitoa picha kwamba Shomary Kapombe beki halisi wa kulia atahamia upande wa kushoto. Hii inakuja baada kumpa mapumziko Nyoni ambaye alicheza ovyo kwenye mechi za kufuzu kombe la dunia dhidi ya Morocco na Ivory Coast.
Huku Uganda ikiwa ndio timu iliyo juu kisoka kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, kocha wa Tanzania alizungumza na kusema yafuatayo."Utakuwa mchezo mgumu sana kwetu kwa sababu Uganda ni timu nzuri; tumekuwa hatuchezi vizuri sana dhidi yao katika mechi za hivi karibuni." 
Wakiwaondoa washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu, ambao wanacheza TP Mazembe ya DR Congo, Taifa Stars itakuwa na wachezaji saba ambao walicheza kwenye mechi za kufuzu kombe la dunia 2014. 
MCHEZAJI WA KUCHUNGWA: Amri Kiemba
Kiungo huyo wa kimataifa wa Simba amekuwa na kiwango kizuri sana kuanzia msimu uliopita kwa Timu yake ya klabu na sasa kwenye timu ya taifa. Ana akili ya mpira, anatuliza mashambulizi na kupeleka mashambulizi kwa adui pamoja kuwatengenezea nafasi wenzie. Ikiwa atacheza kwenye kiwango chake cha juu basi Uganda watapata taabu sana kumchunga Kiemba asiweze kuwadhuru.

TIMU ZINAZOWEZA KUANZA



CRANES  XI (4-2-1-3):
                            Hamuza Muwonge (GK)
Nicolas Wadada - Savio Kabugo - Richard Kasagga - Yusuf Mukisa
                           Hassan Wasswa (Captain) -Dennis Iguma
                                    Joseph Mpande
               Tonny Odur -Patrick Edema - Ronald Muganga
TANZANIA XI (4-3-3)
                             Juma Kaseja (GK)- Captain
Shomari Kapombe - Yondan - Nadir 'Canavaro' Haroub - David Luhende
                           Sure Boy - Frank Domayo
                                   Mwinyi Kazimoto
               Mrisho Ngassa-John Bocco - Amri Kiemba
JE WAJUA ?
- Mpaka kufikia 12th July 2013, Uganda inashika nafasi ya 80 katika listi ya timu bora duniani ya FIFA - wakati Tanzania ikishika nafasi ya 121 na pointi 271.
Uganda Cranes ilifuzu kucheza 2011 CHAN Championships jijini Khartoum, Sudan kufuatia kuifunga Tanzania nyumbani na ugenini.
- Uganda ilifunga goli moja katika CHAN iliyopita iliyofanyika Sudan. Ibrahim Saddam Juma alifunga goli dakika ya 77 dhidi ya Gabon.

- Kocha wa Uganda, atakuwa anaiongoza UG kwa mara ya nne tangu amrithi Bobby,  ameshacheza dhidi ya Libya katika mechi ya kirafiki na kufungwa 3-0, akaja kushinda 1-0 na 2-1 dhidi ya Liberia na Angola katika mechi za kufuzu kombe la dunia 2014.



Tanzania iliwahi kushirikia michuano hii wakati tu ilipoanzishwa na kufanyika nchini Ivory Coast

SIMBA YAIPIGA BAO YANGA - YAMSAJILI HAMIS TAMBWE KWA MIAKA 2


Klabu ya Simba ya Dar es Salaam imefanikiwa kumsajili mfungaji bora wa michuano ya Kagame Cup 2013 Hamis Tambwe kutokea Vital O ya Burundi.

Tambwe ambaye pia alikuwa akiwania na mabingwa wa Tanzania bara Yanga, amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Simba.
Tambwe amesaini mkataba huo mbele ya mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba.