NEYMAR ameanza ufalme wa dunia, itabaki kuwa hivyo mpaka Lionel
Messi na Cristiano Ronaldo watakapochangamsha buti zao kwa mara
nyingine.
Mwanasoka huyo amedhihirisha hilo kwenye Kombe la
Mabara. Michuano hiyo imempandisha daraja na kuonyesha kwamba yupo
sambamba na mastaa hao wawili bora katika Dunia ya soka la kisasa.
Bahati nzuri ni kwamba La Liga, ndiyo
itakayowashuhudia wachezaji wote watatu wakicheza msimu ujao, Neymar
akiungana na Messi katika kikosi cha Barcelona kuendeleza upinzani dhidi
ya Real Madrid inayotawaliwa na Ronaldo.
Kwa kipindi chote za Kombe la Mabara, Neymar
alionyesha kile kilichowafanya Barca wamsajili na kile kilichokuwa
kikiwasukuma Real Madrid wafukuzie saini yake kwa muda mrefu. Wakati
huu, yeye ni namba moja.
Si mchezaji unayeweza kumtumia tu kama mapambo
kwenye majarida na shughuli za kibiashara, Neymar ni mchezaji ambaye ana
uwezo mkubwa wa kuamua matokeo ya mechi na anayesaidia kutwaa mataji.
Alicheza michuano yake ya kwanza mikubwa akiwa na
kikosi cha Brazil kwa usahihi kabisa. Achana na habari kuwa huenda
akachelewa kulifahamu soka la Ulaya, kukosa nguvu au mambo mengine,
Neymar ni fumbo zito kwa Messi na Ronaldo, ambalo kwa sasa wanapaswa
kulifumbua kama wanahitaji kuendelea kuwa juu.
Mbrazili huyo aliwavaa na kuwachachafya wapinzani
wake wa timu zote alizocheza nazo katika mechi tano kwenye michuano ya
Kombe la Mabara. Kiwango chake kwenye mechi ya fainali, dhidi ya
Hispania kilibainisha uwezo wa Neymar ulivyo.
Pasi aliyopiga kwa Oscar kabla ya kufungua nafasi
ambapo kiungo mchezeshaji wa Chelsea alimrudishia tena mpira na kufumua
shuti kwa mguu wa kushoto lililomshinda kipa, Iker Casillas, imeonyesha
Neymar si mchezaji wa kufikirika bali ni halisi.
Neymar hakutaka kucheza na kamera zilizokuwa
zikimmulika kama wengi walivyokuwa wakidhani katika michuano hiyo,
alifanya kazi na kufanikiwa kuipa taji muhimu timu yake.
Wakati filimbi ya mwisho ya michuano hiyo
inapulizwa kwenye Uwanja wa Maracana, Neymar alinyakua tuzo ya Mchezaji
Bora na kuwazima waliokuwa wakibeza kwamba yeye si mchezaji wa mechi
kubwa.
Ikumbukwe kuwa Neymar ndio kwanza ana umri wa
miaka 21, hilo linawafanya Messi na Ronaldo kukuna vichwa. Ni wazi
Ronaldo anapaswa kuweka ‘ubishoo’ kando na Messi afute mawazo ya kwamba
kila kitu ni yeye pale Nou Camp.
Neymar aliingia kwenye gumzo la usajili kwa takribani miaka
miwili iliyopita, hakika huo ulikuwa uamuzi bora wa kuamua kubaki
Brazil mahali ambapo aliweza kujiweka sawa kabla ya kutua Ulaya akiwa
amesogea kwa namna fulani katika kuwanyima raha Ronaldo na Messi.
Uzuri uliopo ni kwamba anakwenda Ulaya katika
mwaka wa kuelekea fainali za Kombe la Dunia, jambo ambalo litampa hamasa
ya kufanya vyema ili awemo kwenye kikosi cha taifa lake la Brazil.
Kutoendelea kucheza nyumbani katika ligi ambayo
haikuwa na ushindani sana ikilinganisha na ligi za Ulaya, kutamsaidia
Neymar kupandisha kiwango chake kiuchezaji.
Sasa kila mmoja anamfahamu Neymar ni nani kwa
kuitazama michuano ya Kombe la Mabara, ambapo Hispania kwenye mechi ya
fainali walishikwa vilivyo na kinda huyo pamoja na umaarufu wao wa
kupiga pasi ndani ya uwanja.
Wakati jina la Neymar likianza kuchomoza, Dunia
bado inaimba majina ya akina Messi na Ronaldo, lakini kwa kuwa Neymar
tayari ametua kwenye bara la Ulaya, kibao kitaanza kubadilika. Sasa
Mbrazili huyo atatawala mazungumzo katika vijiwe vya soka.
Tayari ameshatajwa mara mbili kuwa Mchezaji Bora
wa Mwaka wa Marekani ya Kusini jambo ambalo litamsumbua Messi kwenye
Ballon d’Or ambako amekuwa mtawala kwa miaka minne mfululizo.
Kinachosubiriwa kwa sasa ni kuona Neymar
anaikamata La Liga na Kombe la Dunia 2014 ili aishike rasmi Dunia. Sawa
fedha zimemtoa Brazil na kuhamia Ulaya, lakini uhamisho wake wa
Barcelona unafaida kubwa katika ukuaji wa soka lake na hapo ni mahali
pazuri ambapo ataliweka jina lake katika kurasa za kihistoria.
Kwa vyovyote itakavyokuwa kwa sasa, nyota ambaye
anatazamiwa kuwa gumzo katika fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini
Brazil ni Neymar na si Ronaldo au Messi. Katika klabu ya Barcelona si
kwamba yeye aliitaka timu hiyo bali wababe hao wa Catalan ndio waliotaka
huduma yake, kutokana na hilo ni lazima watamtafutia nafasi ya kuwamo
kwenye kikosi.
Kwa wakati huu, Barcelona inaonekana kuwa ni timu
ya Messi kwa sababu ataendelea kuwa mahali hapo, jambo hilo halimfanyi
Neymar kuonekana si kitu lakini ni wazi kiwango chake kitaanza kumtia
presha Muargentina huyo na umaarufu wake ndani ya Camp Nou.
Akisubiri mwaka mmoja wa taifa lake kuandaa
fainali za Kombe la Dunia, Neymar amepata nafasi ya kucheza kwenye klabu
bora duniani, tena sambamba na wachezaji wajuzi kama Xavi na Iniesta
pamoja na Messi, hilo litamkomaza zaidi katika kufanya mapinduzi ya
utawala katika mchezo huo.
Neymar atakuwa na nafasi ya kufahamu soka la
kimataifa lipoje, si tu Kombe la Dunia, Copa America, Copa Libertadores
na Kombe la Mabara, hapa atapata fursa ya kucheza Ligi ya Mabingwa
Ulaya, ambayo imekuwa ikishirikisha timu bora za klabu na zenye
wachezaji kutoka pande tofauti katika Dunia hii.
Kwa siku za karibuni, Neymar ameweza kuonyesha
kukomaa na si kama ilivyokuwa awali ambapo alikuwa akigongwa kidogo tu
anakwenda chini.
Ukomavu huo wa sasa unaweza kuimarika zaidi wakati atakapojiunga na Barcelona kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.
Presha ya kikosi cha Brazil kwenye Kombe la Dunia
kwa sasa inamhusu Neymar. Tayari ameanza kukomazwa na kuwekwa kwenye
fungu la wachezaji mahiri kama ilivyokuwa kwa Pele, Zico, Ronaldo na
Ronaldinho.
Kizazi kipya cha Brazil kina wachezaji kama Dani
Alves na Thiago Silva, ambao wana uzoefu mkubwa wa kucheza ligi kubwa
barani Ulaya tofauti na Neymar, lakini presha ya kutwaa ubingwa wa Kombe
la Dunia inaendelea kumwandamana kinda huyo.
Kiwango chake cha uchezaji kinapita kwenye hatua
nzuri, swali lililopo je, ataweza kuishinda presha ya Kombe la Dunia?
Kama atafanikiwa kuishinda vita hiyo, hakika atakuwa amewaweka ‘mfukoni’
Messi na Ronaldo
No comments:
Post a Comment