KUNG’ATUKA kwa Sir Alex Ferguson kumeacha vita kubwa kwenye soka juu ya ushindani wa makocha kwamba nani atakuwa bora kwa nyakati zote baada ya Mskochi huyo kuwahi kupachikwa cheo cha ‘Kocha Bora wa Dunia’.
Waswahili wanasema ‘Kila palipo na mwanamume
mwenye mafanikio, nyuma yake kuna mwanamke bora’, hata katika soka ni
hivyo hivyo kwamba, kila kwenye timu yenye mafanikio, nyuma yake kuna
kocha bora.
Mfano ni Manchester City. Ilikuwa na kila kitu,
mabeki wazuri, viungo mahiri na washambuliaji hatari, lakini haikuwa
chini ya mikono ya kocha bora msimu uliopita ilijikuta ikitopoteza taji
lake la Ligi Kuu England kwa timu iliyosaidiwa na kocha bora. Makala hii
inaorodhesha makocha 10 bora wanaoendelea na kazi yao kwa sasa,
wakipangwa si kwa mafanikio yao ya jumla, ingawa yamechukua nafasi yake.
10. Jurgen Klopp (Borussia Dortmund)
Kocha huyo ameingia kwenye orodha hiyo kutokana na
namna alivyoijenga Borussia Dortmund kutoka kwenye timu isiyokuwa na
nguvu sana kwenye ligi, hadi kuwa washindani wakubwa kwenye Ligi Kuu
Ujerumani ‘Bundesliga’ na Ulaya, licha ya kwamba hakuweza kudumu kwa
muda mrefu katika kikosi hicho.
Ubora wa Klopp, si tu kwa kile alichofanikiwa
kukipata, lakini ni kile anachokitarajia kukipata kutokana na namna
alivyouinda timu yake. Kikosi chake cha Borussia Dortmund kiliipoka
Bayern Munich ubingwa wa Bundesliga na hakuishia kulitwaa tu taji hilo
mara mbili mfululizo, bali kuweka rekodi ya pointi kwenye ligi hiyo,
huku akitwaa ubingwa wa Kombe la Ligi bila ya kufanya usajili mkubwa.
Kwa sasa pamoja na Bayern Munich kumnasa nyota
wake, Mario Gotze na Shinji Kagawa aliyehamia Manchester United mwaka
jana, huku Robert Lewandowski naye akiwindwa vikali na timu nyingine,
kwa Dortmund si tatizo kama Klopp ataendelea kubaki.
9. Guus Hiddink (Anzhi)
Kujulikana kwa ubora wake kumetokana na kuzinoa timu za taifa, lakini alifanikiwa kwenye klabu.
Akiwa na PSV Eindhoven, alitwaa mataji matatu
mfululizo ya Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie) kati ya mwaka 1987 na 1989
na alirudia mafanikio hayo katika miaka ya 2003, 2005 na 2006.
Alihamia kwenye soka la kimataifa na pamoja na
kwamba hakuweza kutwaa chochote huko, lakini namna alivyoweza kuzibadili
timu ndogo na kuwa tishio hilo linatosha kuthaminisha ubora aliokuwa
nao.
Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002 alikuwa na
kikosi cha Korea Kusini na kuifikisha nusu fainali timu hiyo kabla ya
kufungwa na Ujerumani. Miaka minne baadaye alihamia Australia na
kuifanya timu hiyo kuwa tishio kwenye Kombe la Dunia 2006 lililofanyika
Ujerumani kwa kuishia raundi ya pili.
Miaka miwili baadaye alikuwa na kikosi cha Urusi na kukifikisha
nusu fainali ya Euro 2008, hapo wakifanikiwa kuwatupa nje Uholanzi na
waliokuwa mabingwa watetezi, Ugiriki kabla ya kutupwa nje na waliokuwa
mabingwa, Hispania. Kwa sasa yupo na kikosi cha Anzhi.
8. Arsene Wenger (Arsenal)
Ameporomoka kidogo tangu zama zile za Arsenal
isiyoshindika, lakini kikosi chake kwa misimu minne mfululizo kimepiku
hatari ya kupitwa na mahasimu wao, Tottenham Hotspur katika msimu wa
Ligi Kuu England.
Baadhi ya mashabiki wanaonekana kuchoshwa na hali
ya Arsenal ya sasa kutokana na kushindwa kuonyesha upinzani, jambo
ambalo linawatisha na kuhofia kuwa kama kilichotokea Liverpool.
Lakini, ukweli halisi, kulingana na sera za timu hiyo, uwepo wa Wenger utaisaidia kuendelea kuwapo kwenye nafasi za juu.
Timu hiyo imekuwa na bajeti isiyoridhisha kwenye
usajili, lakini kwa kulinasa jina kubwa la Gonzalo Higuain , Wenger
anaweza kurejesha makali kwenye timu hiyo kama ilivyokuwa mwaka 1996
alipowasili klabuni hapo.
7. Rafael Benitez (Napoli)
Rafa inaweza kuonekana kama asingeingia kwenye orodha hii baada ya kile kilichotokea Chelsea.
Lakini kutwaa ubingwa wa Ligi ya Europa lililokuwa
taji la pili la Ulaya kwa klabu hiyo ndani ya miaka miwili, hilo
limempandisha chati tangu alipoharibu kwenye nyakati zake pale Inter
Milan.
Kwa ujumla, Rafa amekuwa kocha mwenye mafanikio,
akiweza kuzipandisha Extremadura na Tenerife kucheza La Liga kutoka
daraja la pili, kabla ya kutwaa mataji mawili ya La Liga akiwa na kikosi
cha Valencia, ambapo alivunja utawala wa timu za Real Madrid na
Barcelona zilizokuwa zikipokezana ubingwa.
Baadaye akahamia Liverpool na kuleta mapinduzi
makubwa. Akahama Liverpool na kutimkia Inter Milan, mahali ambako
alikwenda kutwaa Klabu Bingwa ya Dunia, lakini alifanya hivyo akiwa na
timu iliyotengenezwa na Jose Mourinho.
Alirejea England na kujiunga na Chelsea, Rafa
alikumbana na wakati mgumu kutoka kwa mashabiki, akawapa taji la Europa
League kabla ya msimu ujao kuonekana katika benchi la Napoli ya Italia.
6. Vicente Del Bosque (Hispania)
Ingawa ubora wa Del Bosque unatazamwa kwa Hispania
inavyocheza soka lake la kuvutia tangu alipochaguliwa kukinoa kikosi
hicho mwaka 2008, ameng’ara akiwa na msitu wa wachezaji mahiri kabisa
duniani. Lakini umahiri wa Del Bosque haukuanza kuonekana sasa, ilikuwa
hivyo tangu alipokuwa Real Madrid kati ya mwaka 1999 na 2003 ambapo
alitwaa mataji mawili ya La Liga, moja la ligi na mataji mawili ya Ligi
ya Mabingwa Ulaya na jingine la Super Cup.
Hivyo ni wazi kabisa huyo ni kocha bora kabisa
licha ya kwamba hakuwahi kulithibitisha hilo akiwa na kikosi chenye
bajeti ndogo kwenye usajili au timu yenye kiwango cha chini.
5. Pep Guardiola (Bayern Munich)
Jina lake limepata kuwa kubwa baada ya kile
alichokifanya Barcelona, hakika Guardiola ameliteka soka la dunia kwa
staili ya aina yake. Akitumia mwaka mmoja tu kwenye kikosi cha Barcelona
B, kocha huyo alipelekwa kikosi cha kwanza na tangu hapo hakurudi
nyuma.
Alibaki na kikosi hicho kutoka mwaka 2008 hadi
2012, ndani ya miaka hiyo minne, ameweza kutwaa mataji matatu ya La
Liga, matano ya Copa del Rey, mawili ya Ligi ya Mabingwa, mawili ya
Super Cup na mawili ya Klabu Bingwa ya Dunia.
Ubora wake haupo kwenye kutwaa mataji pekee, bali
namna alivyoweza kuifanya Barcelona kucheza soka la gonga za pasi nyingi
na ‘tiki-taka’, mfumo ambao umehamia pia kwenye timu ya taifa na kuweza
kuteka dunia.
Guardiola, 42, aliondoka Barcelona mwaka jana na mwaka huu alitangazwa kuinoa Bayern Munich.
4. Carlo Ancelotti (Real Madrid)
Ancelotti bado anasugua kichwa kujiweka sawa baada
ya kile kilichomkuta Chelsea, mahali ambapo aliondolewa na Roman
Abramovich miaka miwili iliyopita.
Lakini, hilo si la kusumbuka sawa, kwani hata
Roberto Di Matteo aliyefika kwenye timu hiyo na kuipa ubingwa wa Ligi ya
Mabingwa Ulaya, naye amefunguliwa mlango wa kutokea na hakudumu kabisa.
Mwaka huu, ameamua kuondoka PSG na atakuwa mrithi
wa Jose Mourinho katika kikosi cha Real Madrid. Ancelotti ni kocha
mwenye hadhi kubwa, kwa kipindi cha miaka minane aliyokuwa na kikosi cha
AC Milan, amenyakua kila aina ya mataji kwenye kikosi hicho na kuliweka
jina lake juu.
Alipokwenda Chelsea, aliisaidia timu hiyo kunyakuwa mataji
mawili kwa msimu mmoja ikiwa ni mara yao ya kwanza, lakini mwaka
uliofuata wakapigwa kikumbo na Manchester United kabla ya kuondolewa na
Roman Abramovich.
3. Louis Van Gaal (Uholanzi)
Hii ni mara yake ya pili kuwa kocha wa timu ya
taifa ya Uholanzi, lakini ni jambo linalotia masikitiko kwamba mafanikio
yake makubwa kocha huyo ni kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya
akiwa na Ajax mwaka 1995.
Miaka yake aliyokuwa na kikosi hicho cha Ajax, Van
Gaal, aliweza kutwaa mataji kadha, ikiwamo mataji matatu mfululizo ya
ligi, taji la Uefa Cup na Super Cup.
Lakini, tangu alipotwaa ubingwa wa Ulaya, maisha
ya soka la Van Gaal yamepita kwenye nyakati nyingi tofauti, alihamia
Barcelona na kuipa mataji mawili ya La Liga, kisha akatua Bayern Munich
na kuipa Bundesliga na baadaye alirejea Uholanzi kuinoa AZ Alkmaar na
kuwapa ubingwa wa Eredivisie mwaka 2009.
2. Ottmar Hitzfeld (Uswisi)
Kumtaja Ottmar Hitzfeld kwenye orodha hii kunaweza
kuonekana kama masihara kutokana na umri wake, lakini ukweli bosi huyo
atabaki kuwa wa daraja la juu baada ya kile alichokifanya Ujerumani na
Uswisi, ikiwamo ya kutwaa mataji mawili ya Ulaya katika klabu mbili
tofauti.
Aliaza kuipa mafanikio Grasshoppers ya Uswisi kwa
kunyakua mataji mawili ya mfululizo ya ligi na kisha baadaye kuhamia
Borussia Dortmund mwaka 1991.
Ilimchukua Hitzfeld misimu minne tu kunyakua
Bundesliga mwaka 1995 na 1996, wakati huo katika miaka hiyo akitwaa
German Supercup na baadaye akaipa Dortmund ubingwa wake wa kwanza wa
Ulaya mwaka 1997.
Baadaye akahamia Bayern na akaendeleza makali
yake, kabla ya mkataba wake kufika mwisho 2004, alitwaa mataji manne ya
Bundesliga mfululizo, ikiwamo kutwaa mataji mawili kwa msimu mmoja mara
mbili, kisha akaipa taji la Mabingwa Ulaya na kuondoka hapo akiachana
alama zake.
Baadaye Bayern Munich ilimsainisha mkataba
mwingine, ambapo kwenye msimu wake wa mwisho wa 2007-08, aliipa ubingwa
wa ligi kabla ya kuhamia timu ya taifa ya Uswisi.
1. Jose Mourinho (Chelsea)
Alipowasili Real Madrid mwaka 2010, Dunia ilitambua itaona
upinzani mkali katika historia ya soka Hispania baada ya kuwapo
Guardiola katika kikosi cha Barcelona.
Mourinho akabadili kila kitu, akamsumbua Guardiola na utawala wake katika La Liga, kabla ya Mhispania huyo kuamua kuachia ngazi.
Ndani ya uwanja wa soka, Mourinho ni mmoja wa
makocha wenye mafanikio, alitwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara
mbili, akifanya hivyo na FC Porto mwaka 2004 na kisha kurudia akiwa na
Inter Milan mwaka 2010.
Alipohamia Chelsea, Mourinho alijipachika jina la
‘Special One’ na hapo akaweza kuipa timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu
England miaka miwili mfululizo baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka 50
kabla ya kutimkia Inter Milan ya Italia.
Sasa amerejea Stamford Bridge akitokea Real
Madrid, huku kurejea kwake kwa safari hii kukikabiliwa na mtihani mkubwa
wa kufanikisha kile alichoshindwa kukifanya wakati ule, kutwaa taji la
Ligi ya Mabingwa Ulaya na kucheza soka la kuvutia.
No comments:
Post a Comment