BINADAMU wengi wana tabia ya kulewa sifa na hupenda maisha ya kifahari hasa wanapopata fedha nyingi.
Lakini hali ni tofauti kwa mwanasoka nyota wa
Ivory Coast, Yaya Toure, ambaye licha ya kuingiza Pauni 18 milioni kwa
mwaka, hajabadilisha staili ya maisha yake.
Mchezaji huyo ambaye amelelewa kwenye maadili ya
dini ya Kiislamu, amewahi kusema imani yake ndio inamfanya asijione
tofauti na watu wengine licha ya kuwa na fedha nyingi.
Toure ambaye ndugu zake wawili; Kolo na Ibrahim,
nao pia ni wanasoka, amewahi kuanika kuwa hawezi kusahau asili yake.
Jambo hilo ndilo linafanya awe na kawaida ya kutoa vifaa vya michezo kwa
vijana wadogo katika nchi yake na pia kuisaidia familia yake kwa hali
na mali.
“Ninapokuwa mbali na nyumbani, jambo ambaloo huwa nalikumbuka mara zote ni watu wa mji wangu,” alisema.
Maneno yake yanaonyesha jinsi ambavyo mchezaji
huyo hajali maisha ya fedha, anaangalia utu kwanza. Gazeti la Time
lilimtaja mchezaji huyo kushika namba 15 kwa utajiri miongoni mwa
wachezaji wa England.
Mchezaji huyo anashika namba moja kwa kipato kikubwa miongoni mwa wanasoka wa Afrika kwa sasa.
Aliposaini mkataba wa miaka minne wenye thamani ya
Pauni 24 milioni katika klabu yake Aprili mwaka huu, mshahara wake
umemfanya awe kwenye ramani ya wachezaji matajiri. Awali mchezaji huyo
alikuwa akilipwa Pauni 200,000 kwa wiki, lakini baada ya kusaini mkataba
mpya, mshahara wake umekuwa Pauni 240,000 kwa wiki.
Mkataba huo utamfanya aishi Manchester City mpaka mwaka 2017 ambapo wakati huo atakuwa na umri wa miaka 34.
Gazeti la Forbes limemtaja mchezaji huyo kuwa ameshika nafasi ya 67 kwa utajiri miongoni mwa wanamichezo wote duniani.
Ukiachilia mbali matangazo mbalimbali, nyota huyo huweka kibindoni Pauni 5 milioni kila mwaka kwa kipato cha klabuni pekee
Mchezaji huyo ameingia mikataba na makampuni mbalimbali ya
matangazo ya jezi, viatu na haki ya picha ambapo kwa pamoja inamfanya
apate Pauni 11 milioni kwa mwaka.
Vile vile anapata Pauni 823,000 kila wakati Manchester City inapotua kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ingawa mchezaji huyo hapendi makuu, hivi karibuni
alinunua gari aina ya Porsche ya rangi nyeupe ambalo hulitumia
kuzungukia kwenye shughuli zake. Gari hilo lina thamani ya dola 82,050.
Licha ya kuwa na magari yenye thamani kubwa,
anaishi kwenye jumba la kifahari pia huko Cheshire, nyumba hiyo ina
thamani ya Pauni 1 milioni.
Mwanzoni mwa mwaka huu ilidaiwa kuwa nyumba ya
mchezaji huo ilishika moto, hata hivyo kitengo cha zimamoto kiliwahi
kufika eneo la tukio na hakukuwa na madhara makubwa yaliyotokea.
Baba yake alonga
Baba yake (Mory Toure) aliwahi kusema kuwa
anamshukuru Mungu kwa kipato cha mtoto wake ambacho kimewaondoa kwenye
lindi la umasikini.
Mory mwenye umri wa mika 66, ambaye alikuwa
mwanajeshi kabla ya kustaafu, aliwahi kusema: “Kabla watoto wangu (Yaya,
Ibrahim na Kolo) hawajawa nyota katika soka, tulikuwa masikini mno.
“Hatukuwa na uhakika hata wa chakula. Watoto
hawakuwa na mipira ya kuchezea na mavazi yalikuwa ya taabu. Lakini Kolo
na Yaya wameleta mapinduzi makubwa.”
Asilimia 42 ya wananchi wa Ivory Coast wanaishi
kwenye umasikini wa kutupwa. “Nafahamu fedha haziwezi kumfanya mtoto
wangu abadili staili ya maisha. Nadhani fedha hizo zitatumika kumfuta
machozi baada ya kufiwa na mama yake (Tocontoio) wakati alipokuwa na
umri wa miaka 19,” aliongeza baba huyo.
“Ninafahamu hata mke wake (Gineba) anajua nini cha kufanya, hata yeye anaongozwa na sheria za Kiislamu.”
Licha ya kusaidia familia yake, mchezaji huyo anasaidia pia kukuza soka la Ivory Coast na sehemu kadhaa za Afrika Magharibi
Mwaka 2011 aliingia mkataba na kampuni ya vifaa vya michezo ya Puma kwa ajili ya kusaidia chipukizi wa Ivory Coast.
Klabu alizochezea
Yaya Toure aliondoka Ivory Coast akiwa na umri wa
miaka 18 na kuanza soka la kulipwa katika kikosi cha Waasland-Beveren ya
Ubelgiji baadaye akatua FC Metalurh Donetsk ya Ukraine kisha akaenda
Olympiacos F.C. ya Ugiriki.
Baada ya hapo akachezea AS Monaco ya Ufaransa,
hata hivyo mchezaji huyo hakuwa akilipwa vizuri mpaka alipotua Barcelona
mwaka 2007. Mwaka 2010 akatua Manchester City ambapo mshahara wake
ulipanda maradufu.