HABARI zilizopo Dar es Salaam ni kwamba kiraka wa Simba na Taifa
Stars, Shomari Kapombe ameingizwa mkenge kwenye safari yake ya kufanya
majaribio barani Ulaya.
Baadhi ya wadau wamedai wakala anayetaka kumpeleka
mchezaji huyo ni magumashi na kwamba klabu zinazodai kumtaka hazina
mpango naye.
Baadhi ya watu wamenukuliwa wakidai kuwa wakala huyo ni Mtanzania ambaye ametumia ujanja wa kidigitali kumhadaa Kapombe.
Lakini, Kapombe mwenyewe ameitamkia Mwanaspoti kwa
kujiamini kuwa yanayozungumzwa mtaani dhidi yake na wakala huyo ni
uzushi na kwamba ukweli anao yeye na ndio huu anaoueleza hapa.
Kapombe anasisitiza kuwa hakuwahi kuzungumza na
chombo chochote cha habari kuhusiana na safari hiyo na kudai kuwa baadhi
wamekuwa wakimlisha maneno.
Mchezaji huyo ameionyesha Mwanaspoti tiketi yake
ya safari na nyaraka zote za safari hiyo ya Uholanzi Ijumaa ijayo na
tayari ameshalipiwa gharama mbalimbali na wakala huyo aliyemtambulisha
kwa jina la Dionis Kadito ‘Denison’.
“Tayari amelipia gharama za safari ikiwamo tiketi
ya kusafiria, visa na mambo mengine na pia ameahidi kugharamia kila kitu
nitakapokuwa Uholanzi.”
WALIVYOJUANA
Kapombe amelieleza Mwanaspoti kuwa aliwahi
kumsikia wakala huyo kabla ya mwaka jana kukutana naye katika Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam kwenye moja ya mechi za Simba katikaLigi Kuu
Bara.
“Nilikutana kwa mara ya kwanza mwaka jana na
wakala huyu hapa Dar es Salaam na aliniomba tuzungumze kuhusu kufanya
majaribio nje ya nchi,” anasema.
“Licha ya kuwa na ndoto siku moja kucheza soka la
kulipwa, nilitilia maanani walichoniambia kaka zangu kina Boban (Haruna
Moshi) kuwa niwe makini na mawakala wanapokuja, hivyo nikaona nimfuate
mzee wangu wa karibu ambaye ndiye aliyenisaidia Mhadhiri wa Chuo Kikuu
cha Kilimo Sokoine (Sua) kilichopo Morogoro, Profesa Madundo Mtambo
ambaye nilimueleza na nikamwomba anisaidie kujua kamaDenison alikuwa ni
wakala mwenye malengo chanya ya kunisaidia au la.
“Nakumbuka Profesa Mtambo alifanya naye
mawasiliano huku mimi nikiwa kimya na sifanyi naye mawasiliano ndipo
Profesa huyo ambaye ni kama baba kwangu aliponiambia kuwa wakala huyo ni
wa kweli, nimezungumza naye sana na nimefuatilia nyendo zake na kujua
kazi yake kwa ukaribu na ni mtu aliyewasaidia vijana wengine kupata timu
nchi za Ulaya hususani Uholanzi na Ufaransa,” alisema Kapombe akimnukuu
Profesa huyo
Kapombe anasema kuwa aliamua kumtumia Profesa huyo kwa kuwa
amekuwa mshauri wake kwa muda mrefu na amekuwa mpenzi mkubwa wa soka
lake.
Profesa Madundo Mtambo ni mwanasoka msomi na pia
mshambuliaji nyota wa zamani wa klabu ya Reli ya Morogoro na ni
mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine.
WAKUTANA TENA MOROCCO
Kapombe anaeleza kuwa baada ya kuambiwa na Profesa
Mtambo kuwa anaweza kufanya mazungumzo na wakala huyo, ndipo akaanza
kuwasiliana naye kwa ukaribu na akakutana naye tena Morocco akiwa na
Taifa Stars. “Tulipokwenda Marrakech, Morocco tulikutana na
tulizungumza na nikamweleza kuwa sitoweza kwenda kwa wakati huo.
Akanionyesha makabrasha mbalimbali yakiwemo rekodi zake za fedha, barua
kutoka Manispaa ya Jiji ya huko Uholanzi ambayo ni ya kumsaidia kutafuta
visa ya kukaa katika nchi hiyo.
“Pia aliambatanisha taarifa za mtaalamu wa ufundi,
ambaye huwapima wachezaji na kuwasaidia kuwa fiti kabla hawajapeleka
katika timu mbalimbali.”
TIMU ANAZOENDA
Kapombe anasema kuwa amekuwa akisikia watu
wakisema anakwenda FC Twente, lakini wakala huyo alimwambia asiwe na
papara akifika huko ndipo atajua ni wapi atampeleka kufanya majaribio.
“Mimi kwa kweli sijui timu kwa jina ambayo
nitaenda kufanya majaribio zaidi ya wakala huyo ambaye ameniita,
ameniambia kuwa kuna timu mbili, zinazoshiriki Ligi Kuu Uholanzi na moja
ya Ligi Daraja la Kwanza, mimi nahitajika kuweka juhudi zaidi hivyo
timu yoyote itakayovutiwa zaidi kama atakavyosema wakala huyo nitapiga
kazi kwani zaidi naangalia maslahi yangu,” anasema Kapombe.
Dionis Kadito, ambaye ni raia wa Tanzania
anayeishi Uholanzi ni wakala wa wachezaji wa soka anayetambuliwa na
Chama cha Soka Uholanzi na Shirikisho la Soka la Dunia (Fifa).
Kwa mujibu wa Kapombe na baadhi ya makabrasha
yaliyoshuhudiwa na mwandishi wa habari hizi yanaonyesha kuwa Dionis
Kadito anamiliki kampuni inayoitwa DFK Voetbal Agent iliyopo Uholanzi.
SIMBA
Kapombe anasema kuwa mara ya kwanza alipowaeleza
klabu ya Simba mchakato huo: “Waliniambia nitulie lakini mwishowe
walinipa barua, ambayo ndiyo iliyonisaida kwa ajili ya maandalizi ya
safari hiyo kwani bila barua ya Simba ambao ni waajiri wangu nisingeweza
kwenda kokote.
“Simba inaonekana walikuwa wanatazama kwa umakini kama dili
nililopata litakuwa na manufaa kwangu na kwao kama walezi wangu hivyo
nashukuru Mungu walikubali na kunipa baraka zao kufanya majaribio,”
anasema Kapombe ambaye amethibitishwa kwamba mkataba wake na Simba
unamalizika mwakani Aprili na si Desemba kama ilivyokuwa ikidaiwa awali.
“Nahitaji kucheza nje ya nchi, natamani kucheza
ligi nyingine kwani nakusudia kukomaa kiakili na kuwa mchezaji wa
kimataifa,”anasema mchezaji huyo ambaye inadaiwa amewaambia Simba kwamba
hata kama atabaki atataka kucheza zaidi beki ya kulia au kushoto
kwavile ndiko anakomudu zaidi.
Mchezaji huyo wa zamani wa Polisi Morogoro anasema
anapenda kucheza na kujaribiwa kwa nafasi za beki wa pembeni (kushoto
na kulia) na kiungo mkabaji kwani nafasi za beki wa kati hawezi kuzimudu
vizuri kutokana na kimo chake.
“Taifa Stars inanipa faida ya kuonekana, hivyo
nafurahi kuwa kocha huwa ananitumia kwenye hizo nafasi ninazozipenda
ingawa najua kuwa ninapocheza kati huwa nacheza poa lakini ufupi wangu
naona unanipunguzia ubora kwenye nafasi hizo. Pia wakati mwingine mimi
kutumika kama kiraka ina faida zake na zaidi inanigharimu kwa sababu
nabidi kujibadili binafsi na kuvaa uhusika tofauti tofauti,” anasema
Uongozi wa Simba umesema kuwa mchezaji huyo anakwenda kwenye majaribio kwenye klabu ya FC Twente na hawana habari mpya.
No comments:
Post a Comment